Ulega awasimamisha kazi watumishi mizani waliomnyanyasa dereva Pamela




WAZIRI wa Ujenzi, Abdallah Ulega ametangaza kuwasimamisha kazi ili kupisha uchunguzi watumishi wa mizani ya barabara nzima ya kuanzia Tunduma (Songwe) hadi Vigwaza (Pwani) waliokuwa zamu Machi 13 mwaka huu kufuatia kuibuka kwa mvutano kati ya watumishi wa mzani wa Vigwaza na dereva wa magari makubwa ya mizigo aliyefahamika kwa jina la Pamela.

Katika picha mjongeo iliyosambaa kwenye mitandao ya kijamii ilionesha dereva huyo wa magari makubwa ya mizigo ambaye anafanya kazi kwenye kampuni ya Simba Logistics akizungumza na baadhi ya vyombo vya habari, alisimulia alitokea nchini Congo DRC akiwa amepakia mzigo wa tani 32 na Machi 13 mwaka huu  alipofika mzani wa Vigwaza gari lake lilizuiliwa kwa madai kuwa limezidi uzito.

Kufuatia picha hiyo mjongeo, akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma, Ulega ametaja hatua zilizochukuliwa na serikali baada ya yeye kushauriana na menejimenti pamoja na watalaamu mara baada ya Pamela aliyekuwa akiendesha gari lenye namba T137 DLQ na  trela lake T567CUR Pamela kulalamika tabia na menendo ambayo ilijitokeza dhidi yake.

 Ametaja hatua hizo kuwa ni pamoja na kuwasimamisha kazi watumishi hao ili kupisha uchunguzi wa tukio hilo pamoja na kuunda timu itakayofanya uchunguzi kuanzia mahali ambapo gari hiyo iliingia nchini hadi kufika katika kituo cha Vigwaza ambako tukio limetokea.

 Ulega amesema ili kuwa na uchunguzi huru wa mwenendo wa tukio hilo kuwa pia watatazama na mengine yanayoendelea katika mizani hizo nchini na kwamba timu hiyo itahusisha maofisa wa Serikali ambao wanaamini kuwa watafanya kazi kwa haki na kwa weledi mkubwa.

Waziri huyo amewaagiza Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) kubadilisha mifumo ya uendeshaji wa mizani nchini kwa kuwatangazia watu waende na teknolojia ambazo automatic badala ya watu kujadiliana. 

 Katika picha mjongeo, Dereva huyo amefafanua kuwa katika mvutano huo alipobisha kuwa amepita mizani yote na hakukuwa na shida, maofisa waliokuwa kwenye mzani huo walianza kumnyanyasa kuwa asiwafundishe kazi na waliingiza gari kwenye maegesho na kutakiwa kulipa faini ya Sh.956,400 na alipokataa waliendelea kumshikilia bila huduma yeyote.

“Nikamuita mwenye mali akaja na akawaambia wapime ili alipe faini wakasisitiza wao wapo sahihi na mimi nikahoji kwanini ni sahihi wakati mizani mingine nimepita kusiwe na tatizo hapa kwenu kuwe na tatizo? ndipo mtafaruko ukaanza hawakutaka kunisikiliza nikachukua jukumu la kuomba vyombo vya habari vije vinisikilize ili nisikike na mamlaka kama Meneja wa Tanroads, Waziri na Rais asikie kilio cha madereva kwa kuwa mzani huu ni wa mwisho.”

“Nimeanzia mzani wa kwanza ambao ni Mpemba nimepita vizuri, nimekuja Makambako nimepita vizuri, Mikumi nimepita vizuri, Mikese nimepita vizuri nimefika hapa naambiwa mzigo wangu umezidi, sio sawa kutokana na nyaraka nilizonazo na nimeandika barua kwa mamlaka nikaonekana mkaidi, naomba Waziri sisi madereva wa Tanzania hatuthaminiki tunadharaulika na watumishi wa mizani wamekuwa na mtandao ambao wanaweza kukufuata tuyaongee ili tukusaidie, unanisaidia kwenye kitu ambacho si halali je ni haki? Waziri watu wako hawana kauli za kibinadamu, wala za kazi,”amesema.

Amesema ndani ya miezi miwili katika safari yake ya kutoka Kongo na anapofika kwenye mzani wa vigwaza kiongozi wa hapo aliyemtaja kwa jina la Charles anampigia simu na kumkashfu kuwa asiwafundishe kazi kwa kuwa yeye ni mwanamke anatakiwa awe nyumbani hizo ni kazi za wanaume.

“Mimi malalamiko yangu ni kwamba nataka nipime mzani nijihakikishie kwa kuwa walichoniandikia sina uhakika nacho na kama itatokea kupimwa upya naomba waje watu wapya kutoka wizarani wasimame pale kwenye mashine wanipimie na ikiwezekana nisiwe dereva mimi achukuliwe dereva mwingine apime hii gari nijiridhishe na mimi ndio nitakuwa na uhakika wa kulipa, sijakataa kulipa na sijaigomea mamlaka, namuomba Rais aangalie watu wanaomsaidia kwenye Wizara wanamgombanisha na madereva na sisi ndio wapigakura wako,”amesema.

Comments

Popular posts from this blog

TAZAMA HAPA MATOKEO YA KIDATO CHA NNE 2024.

WALIOCHAGULIWA KIDATO CHA KWANZA 2025 MAJINA HAYA HAPA.