Tume huru ya uchaguzi yabaini watu kujiandikisha zaidi ya mara moja

Mkurugenzi wa Uchaguzi Kailima Ramadhani.


TUME Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imesema imebaini uwepo wa changamoto kwa baadhi ya watu kujiandikisha zaidi ya mara moja katika vituo tofauti wakati wa zoezi la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura mkoani Dar es Salaam.

Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo na Mkurugenzi wa Uchaguzi Kailima Ramadhani, huku akibainisha hatua ambazo zinachukuliwa na tume hiyo baada ya zoezi la uandikishaji kukamilika.

Amesema baada ya zoezi la uandikishaji kukamilika katika vituo, tume inachakata taarifa za watu wote walioandikishwa kupitia mfumo maalum wa alama za vidole ambao una uwezo wa kuwabaini wapiga kura wote waliojiandikisha zaidi ya mara moja.

“Kingine tume hufanya zoezi la kulinganisha sura za watu wote walioko kwenda daftari lengo ni kubaini iwapo kuna waliojiandikisha zaidi ya mara moja.

“Pia iwapo itabainika mtu amejiandikisha zaidi ya mara moja, jina na taarifa za mtu huyo, hufutwa na mfumo katika vituo vingine na kubakizwa katika kituo cha mwisho alichojiandikisha katika daftari. Hivyo, taarifa nyingine zote za awali hazitaonekana,” amesema.

Ameongeza kuwa kwa mujibu wa masharti ya kifungu cha 114(1) cha sheria ya uchaguzi wa rais, wabunge na madiwani Na.1 ya mwaka 2024 kujiandikisha zaida ya mara moja ni kosa la jinai na akitiwa hatiani adhabu yake ni faini isiyopungua kiasi cha 100,000 na isiyozidi 300,000.

Amesemaadhabu nyingine ni kutumikia kifungo kwa kipindi kisichopungua miezi sita na kisichozidi miaka miwili gerezani au vyote kwa pamoja, kulipa faini na kifungo gerezani.

Amesema baada ya uchakataji wa daftari kwa mfumo maalumu watakaobainika kujiandikisha zaidi ya mara moja, orodha yao itakabidhiwa kwa Jeshi la Polisi kwa hatua za kisheria.

“Mpiga kura atakayejiandikisha zaidi ya mara moja, mbali ya kutenda kosa anaweza kushindwa kupiga kura kwa kuwa atafutwa katika vituo alivyojiandikisha na kuachwa kituo cha mwisho pengine siyo kituo chake sahihi anachopaswa kupiga kura.

“Tunatoa wito kwa wakazi wa Dar es salaam kuendelea kujitokeza katika siku nne zilizosalia kufikia Machi 23, mwaka huu na tunaendelea kufuatilia zoezi hilo kwa karibu ili kila mwananchi aliyestahili kuandikishwa au kuboresha taarifa zake anapata haki hiyo,” amesema.

Comments

Popular posts from this blog

TAZAMA HAPA MATOKEO YA KIDATO CHA NNE 2024.

WALIOCHAGULIWA KIDATO CHA KWANZA 2025 MAJINA HAYA HAPA.