NEMC:Zifahamu fursa zilizopo kwenye taka
BARAZA la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), limewataka Watanzania kuanza kubadili mtazamo na kuziona taka kama fursa ya kuzirejeleza na kupata bidhaa mbalimbali na kujikomboa kiuchumi.
Kauli hiyo imetolewa jana, jijini Dar es Salaam na Meneja Utekelezaji wa Sheria wa baraza hilo, Amina Kibola, wakati akizungumza na waandishi wa habari.
Amezungumza wakati akizungumzia siku ya kimataifa ya Siku ya Kimataifa ya Kuondoa Taka, ambayo huadhimishwa kila Machi 30 kila mwaka.
Anasema hata kauli mbiu ya mwaka huu, inaweka msisitizo wa kuwa taka si uchafu bali ni malighafi yenye thamani, endapo itasimamiwa na kutumika vyema.

Kibola amesema siku hiyo ilianzishwa rasmi na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Desemba 2022, ili kukuza mifumo endelevu ya matumizi na uzalishaji na kuongeza uelewa kuhusu udhibiti wa taka.
Anasema siku hiyo pia ilianzishwa kwa lengo la kuhimiza mazoea ya kuwajibika ya kupunguza taka ulimwenguni na kwamba kwa hapa Tanzania, watatoa elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa ukusanyaji taka.

“Siku hii inalenga kuhamasisha kupunguza uzalishaji wa taka kwa kutumia dhana ya punguza, tumia tena na rejeleza kwa dhumuni la kuhimiza matumizi bora ya rasilimali zetu, ili kupunguza uchafu na uchafuzi wa mazingira kwa maendeleo endelevu,” anasema.
Amesema kauli mbiu ya siku hiyo kimataifa ni kuwezesha taka sifuri kwenye sekta ya nguo na mitindo na kwamba kwa kuzingatia dhana ya punguza, tumia tena na rejeleza Tanzania, itajenga jamii inayojali mazingira na kuchochea uchumi mzunguko kwa maendeleo endelevu ya taifa letu.
“Kauli mbiu ya kimataifa katika sekta ya nguo na mitindo, inahimiza matumizi ya malighafi zilizo rafiki kwa mazingira, mbinu na ubunifu katika sekta ya mitindo pamoja na viwanda vya kuzalisha nguo, ili kupunguza taka zinazochomwa au kupelekwa kwenye dampo,” amesema.
Ameongeza kwa kusema katika kuadhimisha siku hiyo, NEMC imejipanga kuelimisha, kuhimiza na kuhakikisha kuwa dhana ya punguza, tumia tena na rejeleza katika sekta zote za uzalishaji inatekelezwa kwa vitendo.
Amesema NEMC itahakikisha matakwa ya sheria ya usimamizi wa mazingira katika sekta hiyo yanatekelezwa ipasavyo, ili kuwa na mazingira safi, afya bora kwa jamii na matumizi endelevu ya rasilimali kwa ajili ya maendeleo ya taifa.
“Hivyo basi, (NEMC) kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam inaadhimisha siku hii muhimu katika viwanja vya Mnazi Mmoja, vilivyopo jijini Dar es Salaam.
“Tunawakaribisha wananchi wote kuanzia siku ya Ijuma tarehe 28 hadi tarehe 30 Machi, 2025 kufika, ili kupata taarifa, elimu na kutambua fursa zilizopo katika uwekezaji wa eneo taka za aina zote,” alisema.
Aidha, amesema Machi 30, 2025, ndiyo kilele cha maadhimisho hayo na aliwaomba wananchi na wadau wote kufika viwanja vya mnazi mmoja kuanzia asubuhi hadi jioni, kujionea fursa za uwekezaji katika eneo la taka.
“Wadau zaidi 100 kutoka taasisi za serikali, sekta binafsi, asasi za kiraia na makundi maalum watashiriki na wadau hawa wataonyesha shughuli zao za kila siku ambazo zimelenga kutoa huduma za kukusanya/uzoaji wa taka, pamoja na kurejeleza,” anasema.=
Aidha, amesema wadau hao wanashiriki ili kuonesha wanavyotumia taka kama rasilimali katika kutengeneza bidhaa nyingine, kutoa ajira, kuongeza kipato, kukuza uchumi wa nchi pamoja na kuweka mazingira safi.
“Baraza linahimiza na kuhamasisha wananchi wote waliopo maeneo mengine ya nchi kutumia siku hiyo kwa kufanya shughuli mbalimbali za kuondoka taka kwenye mazingira ili kuendana na dhana halisi ya taka sifuri,” amesema.
“Taka zitenganishwe kwa kuzingatia aina na makundi ili kurahisisha uteketezaji na urejelezaji wa dhana ya punguza, tumia tena na rejeleza mazingira Yetu, Uhai Wetu, Tuyatunze Yatutunze,” amesema
Comments
Post a Comment