Mwalimu Mkuu akamatwa tuhuma za kubaka mwanafunzi Kilosa



Mkuu wa Shule ya Sekondari Zombo, wilayani Kilosa, Mwalimu Mkame Living Mwaisumo (30), anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kumbaka mwanafunzi wa kidato cha pili mwenye umri wa miaka 16.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, SACP Alex Mkama, amesema tukio hilo lilitokea Machi 19, 2025, ndani ya ofisi ya mwalimu mkuu, ambako mwanafunzi huyo alikuwa ameagizwa kupeleka mwongozo wa somo (lesson plan).

Kamanda Mkama alieleza kuwa uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa tukio hilo limetokana na mmomonyoko wa maadili, huku uchunguzi wa kina ukiendelea ili kukamilisha hatua za kisheria dhidi ya mtuhumiwa.

DEREVA ALIYEIBA MAFUTA NA KULICHOMA LORI AKAMATWA

Katika tukio lingine, Jeshi la Polisi limemkamata Abubakar Adam Mwichangwe (29), mkazi wa Tabata Kinyerezi, Dar es Salaam, aliyekuwa akisakwa kwa tuhuma za wizi wa mafuta ya Dizeli lita 35,700 na kuchoma lori alilokuwa akiendesha ili kuonekana kama ajali.

Kamanda Mkama amesema kuwa mtuhumiwa huyo alikamatwa Machi 19, 2025, ikiwa ni siku chache baada ya kutekeleza tukio hilo Machi 16, 2025, ambapo mafuta hayo yenye thamani ya TSh 77,112,000 mali ya kampuni (jina limehifadhiwa) yalikuwa yakisafirishwa kwenda Lubumbashi, DRC kupitia kampuni ya Meru.

Polisi walibaini kuwa dereva huyo alishirikiana na mameneja wa vituo vya mafuta (jina limeifadhiwa) ili kuuza mafuta hayo kisha akachoma lori katika eneo la Misufini, Kilosa, akijaribu kuhalalisha uharibifu huo kama ajali ya moto.

WATUHUMIWA 10 WAKAMATWA KATIKA MSAKO DHIDI YA UJANGILI

Katika hatua nyingine, Polisi kwa kushirikiana na TANAPA wamefanikiwa kuwakamata watu 10 wanaodaiwa kujihusisha na ujangili wa wanyamapori.

Katika msako mkali uliofanyika kati ya Machi 14 - 19, 2025, silaha mbalimbali na viungo vya wanyama vimekamatwa, ikiwa ni pamoja na:
✅ Short gun mbili (2)
✅ Gobole moja (1)
✅ Risasi 22 za shortgun
✅ Maganda 9 ya risasi
✅ Baruti ndogo 2
✅ Vichwa viwili vya mnyama Nsya (Common Duiker)
✅ Miiba 128 ya Nungunungu
✅ Upinde 1 na mishale 4

MAJINA YA WATUHUMIWA WA UJANGILI

🔹 Safari Paschal Tamba (23) – Mkazi wa Tanga
🔹 Jacob Amori Chigange (50) – Mkazi wa Melela
🔹 Mathias John Ndalu (20) – Mkazi wa Melela
🔹 Hussein Rashid (66) – Mkazi wa Melela
🔹 Athuman Robert Matonya (48) – Mkazi wa Vianzi-Mlandizi
🔹 Ismail Omary Mahyoro (75) – Mkazi wa Tandika, Dar es Salaam
🔹 Shaban Mohamed Kalesela (50) – Mkazi wa Mkundi
🔹 Bakari Haruna Nzilie (53) – Mkazi wa Melela-Mlandizi
🔹 Abdulkharim Ibrahim Mashaka (55) – Mkazi wa Kilombero
🔹 Nestory Gabriel Mkami (58) – Mkazi wa Melela-Mlandizi

Polisi wametoa wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana na vyombo vya usalama katika kupambana na uhalifu, ujangili, na vitendo vya mmomonyoko wa maadili, huku wakiahidi kuhakikisha wahusika wa matukio haya wanakabiliwa na mkono wa sheria.


CHANZO: NIPASHE

Comments

Popular posts from this blog

TAZAMA HAPA MATOKEO YA KIDATO CHA NNE 2024.

WALIOCHAGULIWA KIDATO CHA KWANZA 2025 MAJINA HAYA HAPA.