ALAT yawataka madiwani kufanya mikutano ya hadhara

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) Murshid Nzege, (kushoto) akizungumza na waandishi leo kulia ni Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam Omary Kumbilamoto.

Picha Maulid Mmbaga.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) Murshid Nzege, (kushoto) akizungumza na waandishi leo kulia ni Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam Omary Kumbilamoto.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT), Murshid Nzege, amesema sasa ni wakati mwafaka kwa madiwani nchini kuhakikisha wanatoa taarifa kwa wananchi kuhusu maendeleo yaliyofanikishwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, kwa kufanya mikutano ya hadhara kuanzia vitongojini, vijijini, na mitaani.

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam, Nzege amebainisha mafanikio mbalimbali yaliyopatikana tangu Rais Samia aingie madarakani, yakiwemo ujenzi wa madarasa, ajira kwa madaktari na walimu, pamoja na ufanikishaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo. Alisema ni jukumu la madiwani kuwahabarisha wananchi kuhusu utekelezaji wa miradi hiyo.

"Hili litawasaidia wananchi kutambua jinsi Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) inavyotekelezwa kwa vitendo, kwani yapo maendeleo yanayoonekana na mengine ambayo hayajaonekana moja kwa moja, kama vile ajira mpya kwa Watanzania," amesema Nzege.

Akitoa mfano, amesema kuwa katika Halmashauri ya Bukoba, kulikuwa na vijiji 94, lakini wakati Rais Samia anaingia madarakani, vijiji 40 vilikuwa na upungufu wa watendaji. Hata hivyo, hadi sasa, hakuna kijiji kisicho na mtendaji. Aidha, upungufu wa walimu na wahudumu wa afya pia umepungua kutokana na ajira mpya zilizotolewa na serikali.

"Serikali imeenda mbali zaidi kwa kupanga kuhakikisha kila kijiji kinakuwa na mhudumu wa afya aliyepata mafunzo, ili kusaidia jamii husika pale kunapotokea changamoto za kiafya," ameongeza Nzege.

Ameeleza pia kuwa, kwa sasa wananchi wanatoa maoni yao katika halmashauri kwa uhuru zaidi, huku kipato cha wananchi kikiongezeka kutokana na maboresho katika mifumo ya masoko nchini.

Aidha, ametoa pongezi kwa Rais Samia kwa kushughulikia changamoto kubwa ambazo zilikuwa kero katika halmashauri nyingi, ikiwemo ujenzi wa Vyuo vya Ufundi Stadi (VETA) katika kila mkoa, kuboresha stahiki za madiwani, na kuhakikisha malipo ya mishahara kwa wakurugenzi wa halmashauri yanafanyika kwa wakati.

Comments

Popular posts from this blog

WALIOCHAGULIWA KIDATO CHA KWANZA 2025 MAJINA HAYA HAPA.

TAZAMA HAPA MATOKEO YA KIDATO CHA NNE 2024.