Lissu ataka Bunge la dharura kufumua sheria za uchaguzi,.
Vilevile, chama hicho kimetoa mapendekezo matatu kwa serikali kukabili mabadiliko ya kisera kwenye misaada katika sekta ya afya yaliyofanywa na Rais wa Marekani, Donald Trump.
Lissu alisisitiza msimamo huo jana mkoani Dar es Salaam muda mfupi baada ya kukabidhiwa rasmi ofisi katika makao makuu ya chama hicho, Mikocheni, wilayani Kinondoni.
Lissu alisema kuna Uchaguzi Mkuu Oktoba mwaka huu, lakini kwao CHADEMA, kama hakuna mabadiliko, hakuna uchaguzi. Lakini haina maana watasusia uchaguzi.
"Tusijaribu kuitanua lugha kuliko maana yake ya kawaida, hakuna mabadiliko, hakuna uchaguzi. Lazima tuzungumze hayo mambo mawili tuone tunawezaje tukaenda nayo mbele aidha kwa pamoja au kuamua lipi muhimu.
"Sasa hilo sitaki nizungumze hapa, zaidi tunakwenda kujifungia kisha tutaamua kwa pamoja ili uwe uamuzi wa chama na si wangu peke yangu. Tutakwenda kuonana na marafiki zetu duniani tuwaambie msimamo wetu hadharani. Tutawaomba watuunge mkono, na wale wasiotupenda tutawaangalia usoni, tutawaambia msimamo wetu ni huu," Lissu alisema.
Mtaalam huyo wa sheria alisisitiza msimamo huo wa ‘no reforms na election’ siyo wake, bali ni wa chama na kwamba kazi yake ni kutekeleza maagizo ya chama.
Kwa mujibu wa Lissu, chama hicho hakiwezi kwenda kwenye uchaguzi ambao alisisitiza kuwa kuingia katika uchaguzi kwa hali ya sasa ni kukubali kunyolewa au kuwa kama kondoo anayepelekwa machinjioni.
"Tunazungumzia kupata mageuzi kwa shuruti kama walivyopata Kenya, Malawi, Bunge letu linaweza kukaa muda wowote hata bila kuwa na ratiba," alisema Lissu
Alikumbushia kipindi cha nyuma Bunge liliwahi kuitishwa kwa dharura siku ya Jumamosi kuidhinisha Muungano wa Tanganyika na Zanzibar katika ukumbi wa Karimjee, na Muungano mpaka leo upo, hivyo kwa suala la katiba haiwezi kuwa ajabu.
Lissu pia alisema wafuasi wote wa chama hicho watakuwa na haki sawa kulingana na uwezo na kukitumikia chama, na kwamba waliokuwa timu Lissu wasitarajie upendeleo na timu Mbowe kuumizwa, bali wote watakuwa na haki sawa.
Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, John Heche alisema wamejipanga kufanya kazi kikamilifu huku wakilitaka Jeshi la Polisi kuacha kuwatishia kwa kuwa wanatekeleza majukumu yao kwa mujibu wa sheria.
Katibu Mkuu wa CHADEMA, John Mnyika alisema chama hicho chini ya viongozi wapya na wastaafu, watajifungia ndani kwa muda wa wiki moja kwa ajili ya kuja na mkakati wa pamoja kuelekea uchaguzi.
Pia aliwataka wana-CHADEMA kote nchini kuachana na tofauti zilizojitokeza wakati wa uchaguzi na badala yake wasonge mbele kwa nguvu ya pamoja kufanikisha agenda ya mageuzi.
Kuhusu aliyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe kutoonekana wakati wa makabidhiano ya ofisi, Mnyika alisema katiba ya chama hicho inaruhusu Katibu Mkuu kusimamia zoezi hilo na kwamba hakuna shida kama watu wanavyodhani..
Chanzo: Nipashe.
Comments
Post a Comment