CCM yaonya wanaojinadi kabla ya wakati

 



CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), mkoani Katavi, kimewaonya baadhi ya wanachama wake ambao wameanza harakati za chini za kuwashawishi WanaCCM wenzao wawaunge mkono kwenye kinyang'anyiro cha kuwania ubunge katika majimbo ya uchaguzi yaliyopo mkoani humo.

Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Katavi, Iddy Kimanta ametoa onyo hilo kupitia vyombo vya habari hii leo, Desemba 17, 2024 wakati kikao baina yake na waandishi wa habari kilichofanyika kwenye ofisi za CCM zilizopo mjini hapa.

Amesema kwamba zipo taarifa kwamba baadhi ya wanachama wa CCM kwa makusudi wameanza kupita kwa wajumbe na kuwashawishi wawaunge mkono katika harakati zao za kuwania ubunge kwenye majimbo ya uchaguzi yaliyopo katika mkoa huo.

"Wapo WanaCCM kwa makusudi wakijua wanakiuka kanuni, taratibu na miongozo ya Cchama kuhusu kufanya kampeni kabla ya wakati lakini wanafanya hivyo, sasa tunawaonya waache kufanya hivyo mara moja kwa kuwa chama kipo macho, hatutasita kuchukua hatua za kinidhamu kwa wale watakaobainika" alisema

Mwenyekiti huyo, aliongeza kuwa pamoja na watu hao kuanza kampeni mapema lakini pia wanajinadi kwamba wameletwa na baadhi ya viongozi wa juu wa chama na serikali kuja kugombea kitu ambacho sio sahihi.

"Kuna maneno ohoo! kaletwa.....kaletwa nani.....kaletwa," alihoji akiongeza kuwa hakuna biashara hiyo ya mtu kuletwa, huku akikemea tabia ya baadhi ya watu kuwa mafundi wa kutengeneza maneno ambayo yanaweza kusababisha kuondoa umoja na mshikamo uliopo ndani ya CCM katika mkoa huo

Comments

Popular posts from this blog

WALIOCHAGULIWA KIDATO CHA KWANZA 2025 MAJINA HAYA HAPA.

TAZAMA HAPA MATOKEO YA KIDATO CHA NNE 2024.