Kiongozi Mbio za Mwenge asisitiza amani kuelekea Uchaguzi Mkuu

 




Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa, Ismail Ussi, ametoa wito kwa wananchi kuendeleza amani na utulivu kuelekea Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.

Ussi aliyasema hayo alipokuwa akizungumza katika Wilaya ya Rufiji wakati wa ziara ya Mwenge wa Uhuru kwa ajili ya kukagua, kuzindua na kuweka mawe ya msingi kwenye miradi mbalimbali ya maendeleo pamoja na kusambaza ujumbe wa kitaifa wa Mbio hizo.

Aliwahimiza wananchi kuzingatia ujumbe wa mwaka huu unaosema: “Jitokeze kushiriki Uchaguzi Mkuu 2025 kwa amani na utulivu,” akisisitiza kuwa uchaguzi uwe huru, wa haki na wa kumalizika kwa amani kama ilivyopangwa na taifa.

Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Rufiji, Mohamed Mchengerwa, ambaye pia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), alisema kuwa mbio za Mwenge wa Uhuru zimekuwa chachu ya maendeleo nchini kwa kufika katika kila pembe ya Tanzania kukagua na kuchochea utekelezaji wa miradi inayogusa maisha ya wananchi.

“Tutaendelea kupokea maelekezo na mapendekezo ya kuboresha miradi kutoka kwa viongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru, na kuhakikisha kila mmoja anashiriki kikamilifu katika maeneo yote ambayo Mwenge unapita,” alisema Mchengerwa.

Aidha, aliipongeza Serikali kwa kuendelea kuidhinisha fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo, hatua ambayo amesema imeongeza kasi ya maendeleo ukilinganisha na hali ya miaka 60 iliyopita.

Mchengerwa alieleza kuwa Wilaya ya Rufiji imepata mafanikio makubwa katika sekta ya miundombinu, ikiwemo ujenzi wa shule zaidi ya 10, barabara na vituo vya afya ambavyo sasa vimefikia tisa, kutoka viwili tu vilivyokuwepo awali.

Mwenge wa Uhuru katika Wilaya ya Rufiji umetembelea jumla ya miradi sita ya maendeleo yenye thamani ya Shilingi bilioni 1.6, ikiwemo uzinduzi wa bweni la wanafunzi katika Shule ya Sekondari ya Ikwiriri, lenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 80.

Comments

Popular posts from this blog

WALIOCHAGULIWA KIDATO CHA KWANZA 2025 MAJINA HAYA HAPA.

TAZAMA HAPA MATOKEO YA KIDATO CHA NNE 2024.