Trump na Magufuli ni viongozi wa "damu moja" kwa aina yao ya uongozi?

Wapo waliomkosoa na wapo waliomuunga mkono kwa namna alivyozungumza, alivyotoa maamuzi na na maagizo, na jinsi alivyochukua hatua kwa masuala mbalimbali, kwananamna fulani ya ufanano kama ilivyo sasa kwa Rais Donald Trump wa Marekani, ambaye wapo wanaomkoa na wapo wanaomuunga mkono kwa anayoyazungumza na kuyatenda.
Baadhi ya watu wanawafananisha kwa kiasi kwa namna wanavyotawala na kuongoza mataifa yao, licha ya tofauti kubwa iliyopo kati ya Tanzania na Marekani kwenye eneo la uchumi, siasa, huduma za kijamii na hata idadi ya watu. Marekani ikiiacha mbali Tanzania kwenye kila eneo.
Ingawa viongozi hao waliongoza mataifa yenye historia, tamaduni, uchumi, na siasa tofauti, wote wanashabihiana kwa masuala kadhaa, kuanzia mtindo wa uongozi hadi maamuzi yao yenye utata. Makala hii inachambua mambo saba yanayoleta mfanano wa namna wanavyotawala na kuendesha serikali zao, bila kuzingatia iwapo wanapatia ama wanakosea.
1. Viongozi wa wananchi kwanza

Magufuli kama ilivyo kwa Trump alijitambulisha kama mpinzani wa mfumo wa kisiasa uliokuwepo ambao kama uliwasahau ama unawasahu watu wa hali ya chini ama wananchi wa nchi husika. Wote walijenga umaarufu wao kwa kupinga kile walichokiita "mfumo wa kifisadi" au "deep state," na kujitokeza kama watetezi wa wananchi wa kawaida. Magufuli akijinasibu kama mtetezi wa wanyonge, Trump akijinasibu kama mtetezi wa wamarekani wa kawaida.
Magufuli alipoingia madarakani mwaka 2015, alianza kwa kampeni kali ya kupambana na ufisadi, akiwafukuza watumishi wa umma hadharani. Mfano mzuri ni Desemba 2015, alipoamuru kufukuzwa kwa viongozi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa madai ya upotevu wa mabilioni ya fedha za serikali. Hakutaka kodi za wananchi zipotee kihohela kwa namna alivyoona yeye. Akiwaondoa pia aliowaita wafanyakazi hewa na waliotuhumiwa kuwa na vyeti ghushi vya kidato cha nne.
Trump kwa upande wake alipoingia Ikulu ya Marekani mwaka 2017, alitangaza kuwa anakuja "kusafisha mfumo wa Washington" na mara nyingi aliwashambulia viongozi wa chama chake cha Republican, akiwaita sehemu ya tatizo. Katika awamu yake ya pili ya utawala iliyoanza Januari 2025, tunamuona Rais Trump akiwaondoa maelfu ya wafanyakazi, akifunga misaada ya kijamii ambayo Marekani ilikuwa inatoa kwa nchi zinazoendelea kupitia shirika lake la USAID.

2. Maamuzi ya kushangaza ya papo kwa hapo
Kama kuna mahali watanzania wanamkumbuka zaidi Magufuli, ni eneo la kutoa maamuzi ya papo kwa hapo kwenye mikutano ya hadhara, na mara nyingi bila kujali athari zake kwa muda mrefu.
Kwa mfano Machi 2017, bila onyo lolote, aliamuru kufungwa kwa maduka ya kubadilisha fedha za kigeni nchini Tanzania kwa madai kuwa yalihusika na utakatishaji wa fedha. Trump anafanya hivyo kupitia amri za rais anazozitoa kila leo.
Trump yeye mnamo Juni 2018, aliamua Marekani ijitoe kwenye Mkataba wa Nyuklia wa Iran (JCPOA), licha ya upinzani mkubwa kutoka kwa washirika wa Marekani kama Ufaransa, Ujerumani, na Uingereza.
Kuna wakati inatajwa aina ya maamuzi yao yanaegemea kwenye kujijenga kwa sifa kadha wa kadha. Ilionekana hivyo wakati wa Magufuli, ambapo asilimi kubwa ya vyombo vya habari viliripoti na kumsifu yeye na mambo anayoyafanya ikiwemo miradi mbalimbali. Wanaomuunga mkono wakiwemo mawaziri na watumishi wa serikali walilazimika kuimba 'wimbo' mmoja wa kumpa sifa zake. Inaonekana hivyo kwa Trump pia kwa sasa.
3. Uongozi wa Mkono wa Chuma

Uongozi wa Mkono wa Chuma (Authoritarian Leadership Style) unahusu viongozi wanaoamini katika mawazo yao zaidi na ukionekana kuyapinga unajiweka matatani.
Licha ya kuendesha nchi zilizo na mifumo tofauti ya utawala, wote wawili walituhumiwa kwa kutumia mbinu za kimabavu dhidi ya wapinzani wao. Kwa mfano Trump ametoa amri ya kuwapa likizo wafanyakazi wote wa Shirika la Utangazaji, maarufu Sauti ya Amerika (VOA), linaloonekana kumpinga na kupinga mengi katika utawala wake.
Magufuli alifanya hivyo, ingawa hakuligusa Shirika la utangazaji Tanzania (TBC), lakini alivionya kwa ukali vyombo vya habari vilivyokuwa vinamkosoa kwa uwazi. Pengine ni kwa sababu TBC haikufanya chochote ambacho kingetafsiriwa na Magufuli kuwa ukosoaji.
Novemba 2016, uongozi wa Magufuli ulilifungia gazeti la Mawio kwa miaka miwili kwa tuhuma za kuchapisha habari zilizoleta "uchochezi" kuhusu siasa za Zanzibar. Mwaka huo wa 2016 wakati akitimiza mwaka mmoja madarakani, alisisitiza na kuwaonya wamiliki wa vyombo vya habari kuwa kuna uhuru wa habari, lakini "uhuru huo una mipaka."
"Nawaambia wamiliki wa vyombo vya habari, "be careful," (chukueni tahadhari), "watch it" (angalieni) kama mnafikiri mna freedom ya namna hiyo "not to that extent" (sio kwa kiwango hicho)", Ilikuwa kauli tata iliyopokewa kwa ukosoaji mkubwa ndani na nje ya nchi. Waliomkosoa wakiona kama anavitisha ili asipingwe na kukosolewa, na kwa kufanya hivyo alikuwa anaminya uhuru wa habari.
4: Demokrasia ya 'ukakasi' katika mikono yao

Marekani ni nchi mama kwenye demokrasia duniani. kwa miaka mingi imekuwa mfano linapofika suala la demokrasia. Lakini Trump alitikisa uhalali wa demokrasia ya Marekani baada ya kupinga matokeo yaliyompa ushindi Joe Biden katika uchaguzi wa 2020. Trump amekuwa akitumia mitandao kama X zamani Twitter kwa mtindo mkali wa kisiasa.
Mfano ni mwaka 2020, aliposema kuwa uchaguzi wa Marekani ulikuwa "umeibwa," kauli ambayo ilichangia ghasia za wafuasi wake katika majengo ya Bunge la Marekani mnamo Januari 6, 2021
Ilisababisha uharibifu mkubwa. Lilikuwa tukio la ajabu.
Kwa upande wa Magufuli, uchaguzi wa serikali za mitaa 2019 ulikuwa wa aina yake ambapo wagombea wengi wa upinzani waliondolewa kama ilivyokuwa kwa uchaguzi mkuu wa 2020. Wanaokosoa wanaona Magufuli alikuwa tishio kwa Demokrasia ya Tanzania ambayo ilianza kuonekana kwenye ramani ya dunia kuwa yenye kupiga hatua.
5. Ushirikiano wa Kimataifa

Hapa kuna eneo wanalingana na kuna mahali wanatofautiana kiasi. Japo Magufuli hakupenda kufanya ziara nje ya nchi kuimarisha mahusiano, na ziara chache alizofanya alizifanya barani Afrika, Trump angalau anatoka. na Asipotoka anawakilishwa na uwepo wake unaonekana kupitia uwakilishi huo. Ukweli Magufuli kama ilivyo kwa Trump wanaonekana kuwa na tahadhari kubwa kuhusu mikataba ya kimataifa, wakiona kuwa mingi ilikuwa ya kinyonyaji kwa nchi zao.
Kwa mfano, mwaka 2017, Magufuli alikataa mkopo wa $10 bilioni kutoka China kwa ajili ya mradi wa bandari ya Bagamoyo, akidai masharti yake yalikuwa ya kinyonyaji kwa Tanzania.
Novemba 2020, Tanzania ilithibitisha kujiondoa rasmi kwenye kipengele cha Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu (AfCHPR) kinachoruhusu watu binafsi na mashirika yasiyo ya kiserikali kuishtaki Serikali baada ya kupita mwaka mmoja tangu ilipoandika kusudio la kujiondoa chini ya Rais Magufuli.
Trump kwa upande wake, Juni 2017, alitangaza kujitoa kwenye Mkataba wa Hali ya Hewa wa Paris, akisema ulikuwa unaiumiza Marekani kiuchumi huku ukiwanufaisha mataifa mengine. Marekani chini yake ikatangaza kujitoa kwenye Baraza la Umoja wa Mataifa la Haki za Binadamu huko Geneva kwa tangazo la aliyekuwa Waziri wa Mambo ya nje, Mike Pompeo na Balozi wa Marekani kwenye Umoja wa Mataifa, Nikki Haley.
Mawazo yake kuhusu ushiriki wa Marekani katika Shirika la afya duniani (WHO) linakwambia Trump ni mtu wa aina gani.
6. Tumbua tumbua ya 'fedheha'

Wote wana mamlaka kama marais kufanya maamuzi ya kuondoa watumishi walioonekana wazembe ama watumishji wasioendana na mifumo yao ama walichokitaka. Lakini wakosoaji wanawatizama kama wanaotumbua ama kuwaondoa watumishi kwa njia isiyo 'staha' ya kuwalindia heshima na utumishi wao.
Trump si muumini wa mfumo wa kisiasa wa Kawaida (Anti-Establishment Stance), kama ilivyokuwa kwa Magufuli. Kuna wakati walivunja taratibu za kisiasa za kawaida na kupambana hata na viongozi wa ndani ya serikali zao.
Kwa mfano Magufuli aliwatimua ama ' kutumbua' maelfu ya wafanyakazi wa serikali kwa madai kuwa walikuwa na vyeti ghushi, akisema hana muda wa kupoteza na watu wasiostahili kuwa serikalini, alisema hadharani na wengine walitumbuliwa hadharani.
Trump yeye mara kwa mara alikosana na maafisa waandamizi wa serikali yake na kuwaondoa kwa mtindo unaokosolewa. Mfano halisi ni mnamo 2018, alipomfukuza kazi Waziri wake wa Mambo ya Nje, Rex Tillerson, kupitia ujumbe wa Twitter. Wapo wafanyakazi wanaotimuliwa sasa kwa kutumia barua pepe, chini ya kitengo cha ufanisi wa shughuli za serikali (DOGE) anachokisimamia bilionea Elon Musk.
7. Maamuzi magumu

Magufuli aliamini sana juu ya maamuzi yake, licha ya mengine kuwa ya 'utata'. Alifanya maamuzi magumu mengi ukiacha kutumbua na kukinzana na wakubwa wa nje kupitia mikataba mbalimbali ikiwemo ya madini. kwa mfano kujenga bwawa la umeme la Julius Nyerere (JNHHP) ambao ulikosolewa na watetezi wa mazingira leo unaingiza karibu robo tatu ya umeme kwenye gridi ya taifa ya Tanzania.
Pia mradi wa treni ya kisasa (GSR) na kusitisha mradi wa bandari ya Bagamoyo, ulikuwa uamuzi ni ushahidi wa namna alivyoweza kufanya maamuzi yaliyoonekana magumu kwa wengine.
Machi 2020, alipinga masharti ya Shirika la Afya Duniani (WHO) kuhusu COVID-19, akisema Tanzania haitafunga uchumi wake kwa sababu ya ugonjwa huo. Alikwenda mbali zaidi kwa kudai kuwa hata papai lililopimwa na maabara lilionekana kuwa na virusi vya corona. Uamuzi ambao ulikuwa mgumu kufanyika na viongozi wa mataifa mengine, ambayo mengi yalifunga nchi zao kutokana na corona.
Kuhusu vita vya Ukraine, Gaza, na kuongeza ushuru kwa bidhaa za nje ikiwemo China, Ulaya na Asia, ni uamuzi ambao si rahisi kuufanya kwa kiongozi asiyeamini kwenye maamuzi yake na athari zake kwa wengine. Trump ameufanya. Aidha ushahidi mwingine ni Februari 2017, alipokosoa hadharani mashirika makubwa ya kiusalama, lile la upelelezi (FBI) na la ujasusi (CIA), akidai kuwa taasisi hizo zilikuwa zinampinga kwa sababu ya ajenda zake mpya.
kwa hiyo, utawala wa kiimla, upinzani dhidi ya mfumo wa kisiasa wa jadi, na maamuzi yenye msimamo mkali yatabaki kama masuala mengi ya kukumbukwa kwa Magufuli.
Historia itawahukumu Magufuli na Trump kwa namna tofauti, lakini jambo moja ni wazi: Magufuli kaacha alama ya kwenda tofauti na taratibu za kawaida zilizozoeleka, jambo ambalo Trumpa analipitia sasa.
Ameacha alama isiyoweza kufutika katika siasa za Tanzania na Afrika, na Trump bila shaka ataacha alama kwa dunia.
Comments
Post a Comment