CHADEMA kutinga mahakamani kushtaki INEC
MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, amesema chama hicho kwa kushirikiana na wadau wengine, kiko kwenye mchakato wa kwenda mahakamani kuishtaki Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC).
Lissu, mtaalam wa sheria na mbunge wa zamani wa Singida Mashariki, amesema lengo lao ni kuzuia mchakato wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, ukiwamo ugawaji majimbo uliotangazwa hivi karibuni na INEC.
Alibainisha hayo jana wakati wa mahojiano maalumu na waandishi wa habari wa gazeti la Nipashe na Nipashe Digital, nyumbani kwake Tegeta mkoani Dar es Salaam.
Lissu alisema tayari mchakato huo uko tayari na wakati wowote watakwenda mahakamani.
"Kwanza kwenye hiyo ya tume kuanza mchakato wa kutengeneza majimbo upya, tunafungua kesi Mahakama Kuu kwa kushirikiana na wadau wengine kama Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS), na mimi nimesaidia kudrafti hiyo kesi, kuomba itamke kwamba huo mchakato ni haramu, iupige marufuku.
"Ni haramu kwa mujibu wa Katiba ya nchi yetu, utaratibu wa kutengeneza majimbo ya uchaguzi ni wa ovyo sana na unasema tume inapotaka kutengeneza majimbo ya uchaguzi, inatakiwa kuangalia vigezo viwili tu, kuwapo miundombinu na jiografia, haiangalii binadamu kwa ajili gani, ina uhusiano gani na uchaguzi... Mungu anajua, waliotunga Katiba yetu watueleze.” alisema Lissu
Comments
Post a Comment