Taharuki yatanda meli kutitia bandarini

 



TAHARUKI ilitanda kwa wakazi wa Mwanza baada ya kuwapo taarifa kuwa meli ya MV. Serengeti, imetitia upande wa nyuma na kuzama ziwani ikiwa imeegeshwa katika bandari ya Mwanza South.

Tukio hilo limetokea zikiwa zimepita siku 222 baada ya meli ya MV. Clarias kupinduka na kuanguka majini ikiwa imeegeshwa katika bandari ya Mwanza North.

Taarifa za kutitia kwa meli hiyo yenye uwezo wa kubeba abiria 500 na tani 250 za mizigo, zilienea juzi katika mitandao ya kijamii kwamba imezama ikiwa na mizigo.

Akizungumza na mwandishi wa habari hii eneo la bandari hiyo, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Meli Tanzania (TASHICO), Wakili Alphonce Sebukoto, alikiri kutitia kwa meli na kusema haikuwa na safari yoyote tangu mwaka 2016.

Sebukoto alisema walipata taarifa kutoka kwa walinzi wa eneo hilo juu ya meli hiyo kutitia na sehemu ya nyuma kuanza kuzama usiku wa kuamkia Desemba 26, majira ya saa 7:00 usiku, hivyo kutuma wataalamu kuanza juhudi za kuiinua.

Alisema meli hiyo ni miongoni mwa meli nne ambazo haziko kwenye uendeshwaji na zimeegeshwa katika bandari hiyo inayotumika kuegesha meli ambazo zinasubiri matengenezo.

“Si kweli kwamba meli hii ilikuwa na mizigo bali tangu mwaka 2016 imeegeshwa kwa ajili ya kufanyiwa matengenezo makubwa. Kilichotokea  ni maji kuingia ndani ya meli kwa nyuma na kuanza kuzama majini, hivyo wataalam wetu kwa kushirikiana na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji upande wa majini, wanaendelea na jitihada za kuiondoa ili uchunguzi wa chanzo uanze,”alisema Wakili Sebukoto.

Pia alisema baada ya kuinuliwa itapandishwa kwenye chelezo ambako watachunguza kujua sababu ya maji kuingia ndani ya meli hiyo ambayo imetengenezwa mwaka 1988 na imekaa bandarini hapo kwa miaka tisa.

UCHUNGUZI MV.CLARIAS

Kuhusu uchunguzi uliotangazwa kuanza kufanyika tangu Mei, mwaka huu,  ilipozama meli ya MV. Clarias muda mfupi baada ya kutoka kwenye safari zake,  Sebukoto alisema matukio hayo yana tofauti.

Alisema kutokana na kuwa meli hiyo haikuwa na tatizo lolote na ilikuwa inaendelea na safari, uchunguzi unaendelea kupitia kamati ya ulinzi na usalama ili kubaini kama ajali hiyo ilitokea bahati mbaya au makusudi.

“Ilibainika kuwa matundu maalum ya kuruhusu meli kupumua ‘stern tube’  yalikutwa na upana usio wa kawaida hali iliyoruhusu maji kuingia kwa wingi na kusababisha uzito kuegemea upande mmoja.  Tatizo  hilo linaweza kusababishwa na ama  maji kuingia au kushushwa kwa mkono wa binadamu,” alisema Sebukoto.

Pia alisema taarifa kuhusu jambo hilo zitatolewa mara baada ya uchunguzi na ikibainika kuna uzembe au hujuma uliyofanyika  wahusika watafikishwa mahakamani kwa kuwa serikali haiwezi kuvumilia kuona vyombo vyake vikihujumiwa.

Katika kuhakikisha matukio hayo hayajirudii, alisema TASHICO ina mpango wa kuweka mifumo ya kiusalama ya kidijitali zikiwamo kamera ili pale linapokaribia kutokea tukio la namna hiyo, lidhibitiwe mapema.

“Hizi meli zetu zimetengenezwa katika mifumo ya zamani, hivyo hazina ‘alarm’ ambazo zinasaidia kutambua tatizo endapo maji au moshi usiohitajika ukiingia. Pia  hazina kamera, hivyo mpango ni kufunga vitu hivyo ili kutoa taarifa mapema,” alisema.

Akizungumza wakati wa uokoaji wa meli hiyo, Kiongozi wa Kitengo cha Uokoaji Ndani ya Maji kutoka Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Mwanza, Mkaguzi Msaidizi Said Sekibojo, alisema hakuna madhara yaliyopatikana kwenye chombo hicho na taratibu za kukitoa majini zinaendelea.

“Kazi kubwa tunayoifanya ni kuifunga na kuanza kuinyanyua, kisha kumwaga maji ambako tunaendelea hatua hiyo na kufikia leo (jana) jioni tunatarajia kuwa tumekamilisha kila kitu,” alisema Sekibojo

Comments

Popular posts from this blog

WALIOCHAGULIWA KIDATO CHA KWANZA 2025 MAJINA HAYA HAPA.

TAZAMA HAPA MATOKEO YA KIDATO CHA NNE 2024.