SIFA NA VIGEZO VYA KUJIUNGA NA J K T HIVI HAPA

JESHI la Kujenga Taifa (JKT), limetangaza nafasi za vijana kujiunga na mafunzo ya jeshi hilo kwa kujitolea kwa mwaka 2024 huku likitoa tahadhari ya matapeli wanaoomba fedha ili kuwatafutia nafasi jeshini.
Akizungumza na waandishi wa habari jana kwa niaba ya Mkuu wa JKT, Kaimu Mkuu wa Tawi la Utawala wa JKT, Kanali Juma Mrai, alisema utaratibu wa vijana kuomba na kuchaguliwa kujiunga na mafunzo hayo unaratibiwa na ofisi za wakuu wa mikoa na wilaya katika eneo analotoka mwombaji.
Alisema usaili wa vijana hao kujiunga na mafunzo hayo ya kujitolea umepangwa kuanza Oktoba 2024 kwa mikoa yote ya Bara na visiwani na watakapochaguliwa wataripoti kwenye kambi za jeshi kuanzia Novemba 1 na 3, 2024.
“Kumekuwa na wimbi la utapeli unaoendeshwa na baadhi ya watu ambao wakiwaomba fedha vijana wanaoomba nafasi hizo, naomba niwaambie nafasi hizi haziuzwi ni bure hivyo kila mmoja aombe sehemu husika zilizotolewa na JKT,” alisema.
Aidha, alisema vijana hao ambao watachaguliwa kujiunga na mafunzo hayo, JKT haitoi ajira pia haihusiki kuwatafutia ajira katika asasi na vyombo mbalimbali vya ulinzi na usalama bali jeshi hilo hutoa mafunzo kwa ajili ya kuwaandaa vijana kwa ajili ya kujiajiri wao wenyewe.
Alibainisha sifa za waombaji wa nafasi hiyo kuwa ni vijana wa darasa la saba wanapaswa kuwa na umri kuanzia miaka 16 hadi 18 ambao wamemaliza elimu ya msingi kuanzia mwaka 2021, 2022 hadi 2023 wawe na cheti cha kumaliza elimu ya msingi.
Pia, alisema kwa vijana waliohitimu kidato cha nne kuanzia mwaka 2021, 2022 hadi 2023 wanapaswa kuwa na umri usiozidi miaka 20 na awe na ufaulu kuanzia daraja la kwanza hadi la nne na ufaulu uwe kuanzia alama 26 hadi 32.
Pia, alisema kwa waliohitimu kidato cha sita wawe na umri usiozidi miaka 22 ambao wamemaliza kuanzia mwaka 2021, 2022, 2023 na awe na cheti chenye ufaulu wa kuanzia daraja la kwanza hadi la nne.
“Vijana wa Stashahada umri usiwe zaidi ya miaka 25, wale wa shahada umri usiwe zaidi ya miaka 26 na wenye shahada ya uzamili umri usiwe zaidi ya miaka 27,” alisema.
Comments
Post a Comment