Kiongozi Mbio za Mwenge asisitiza amani kuelekea Uchaguzi Mkuu
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa, Ismail Ussi, ametoa wito kwa wananchi kuendeleza amani na utulivu kuelekea Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu. Ussi aliyasema hayo alipokuwa akizungumza katika Wilaya ya Rufiji wakati wa ziara ya Mwenge wa Uhuru kwa ajili ya kukagua, kuzindua na kuweka mawe ya msingi kwenye miradi mbalimbali ya maendeleo pamoja na kusambaza ujumbe wa kitaifa wa Mbio hizo. Aliwahimiza wananchi kuzingatia ujumbe wa mwaka huu unaosema: “Jitokeze kushiriki Uchaguzi Mkuu 2025 kwa amani na utulivu,” akisisitiza kuwa uchaguzi uwe huru, wa haki na wa kumalizika kwa amani kama ilivyopangwa na taifa. Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Rufiji, Mohamed Mchengerwa, ambaye pia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), alisema kuwa mbio za Mwenge wa Uhuru zimekuwa chachu ya maendeleo nchini kwa kufika katika kila pembe ya Tanzania kukagua na kuchochea utekelezaji wa miradi inayogusa maisha ya wananchi. “Tu...