Mtoto wa Osama Bin Laden atakiwa kuondoka nchini Ufaransa
Serikali ya Ufaransa imemuamuru Omar bin Laden, mtoto wa kiongozi aliyeuawa wa Al Qaeda Osama bin Laden, kuondoka nchini humo kutokana na machapisho yake kwenye mitandao ya kijamii. Waziri mpya wa mambo ya ndani wa Ufaransa Bruno Retailleau, ameandika kwenye mtandao wa X kwamba mtoto huyo wa Bin Laden alichapisha mwaka jana maoni kwenye mitandao yake ya kijamii ambayo yalitetea vitendo vya ugaidi.Omar mwenye umri wa miaka 43, alizaliwa na kuishi nchini Saudi Arabia kabla ya kuelekea katika mataifa ya Sudan na Afghanistan. Alijitenga na baba yake akiwa na umri wa miaka 19 na akaamua kuishi na mke wake raia wa Uingereza huko Normandy kaskazini mwa Ufaransa mnamo mwaka 2016 akijishughulisha pia na uchoraji. Swahili.